Mchungaji wa Kanisa la Maombezi (GRC) la Ubungo Kibangu, Anthony
Lusekelo, amesema Chama Cha Mapinduzi (CCM), kinashinikiza kusainiwa kwa
Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa mwaka 2013,
ili ipatikane katiba itakayokibeba chama hicho.
Wakati Lusekelo akieleza hayo, Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gosper
Bibble Fellowship (FGBF), Zacharia Kakobe, amesema kuwa diwani, mbunge,
waziri na rais haina maana kuwa una mamlaka yote dhidi ya Watanzania.
Mchungaji wa Kanisa la Maombezi (GRC) la Ubungo Kibangu, Anthony Lusekelo |
Kauli za viongozi hao wa dini, zimekuja
katika kipindi ambacho vyama vya siasa, wanaharakati na wananchi
wamekuwa wakimshinikiza Rais Jakaya Kikwete, kutosaini muswada huo na
badala yake, urejeshwe bungeni, ili ukafanyiwe marekebisho kwa maelezo
kuwa una kasoro nyingi.
Akizungumza na chanzao cha habari hii Lusekelo maarufu kama ‘Mzee wa
Upako’ alisema CCM inatambua kuwa mapendekezo yaliyomo katika Rasimu ya
Katiba kama yakipita, chama hicho kitakuwa katika wakati mgumu, hivyo ni
lazima kihakikishe kuwa hatua hiyo inakwama.
“Hiki chama kinaweza hata kung’oka madarakani kama mapendekezo ya sasa
yatapita. Namshauri Rais Kikwete asikilize malalamiko ya Watanzania
kuhusu muswada huu, asisaini na aurudishe bungeni ili ufanyiwe
marekebisho,” alisema na kuongeza kuwa;
Kitendo cha wabunge wa chama kimoja kuwa wengi katika Bunge la Katiba,
Zanzibar kutokushirikishwa katika utoaji wa maoni na Tume ya Mabadiliko
ya Katiba kumaliza majukumu yake baada ya kukabidhi rasimu katika Bunge
la Katiba, ni kasoro kubwa zilizoibuliwa na wanasiasa lakini zikapuuzwa.
Mbali na kuiponda sheria ya mabadiliko ya katiba, Lusekelo alisema
lingekuwa jambo la busara kama Bunge la Katiba lingekuwa na wajumbe
ambao sio wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kwa upande wake, Askofu Kakobe wakati akizungumza katika ibada ya misa ya pili kanisani kwake
Mwenge Dar es Salaam, alisema viongozi
wa nchi wamechaguliwa kwa neema ya Mungu, wasitumie nafasi zao kuamua
kila jambo hata kama halina maslahi kwa nchi na wananchi wanaowaongoza.
“Viongozi wanatakiwa kuacha kujigamba na
kujiona wao ni kila kitu, nafasi walizonazo ni dhamana tu na siku moja
Mungu anaweza kuwanyang’anya na kuwapa wengine,” alisema kiongozi huyo
wa kidini.
Source:mwananchi
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni