Meriam akiwa na watoto wake.
Mwanamke aliyekuwa amehukumiwa kifo kabla ya kuachiwa huru hivi majuzi Meriam Ibrahim wa nchini Sudan ameeleza kwamba kitendo cha kujifungua mtoto wake akiwa gerezani ilihali miguu yake ikiwa imefungwa minyororo imemsababishia mtoto wake apate ulemavu.
Meriam ameyaeleza hayo wakati akihojiwa na gazeti la The Guardian la nchini Uingereza kwamba ilikuwa vigumu kwake katika kujifungua binti yake aliyempa jina la Maya kwakuwa miguu yake ilikuwa imefungwa minyororo ndani ya gereza la wanawake la Omdurman lililopo kaskazini mwa jiji la Khartoum nchini humo. Meriam amesema kwamba alilazimishwa kujifungua akiwa katika hali hiyo jambo ambalo lilisababisha kujifungua binti yake kwa shida na kumsababishia ulemavu wa mwili na kwamba amesema hajui endapo Maya atakuwa na uwezo wa kutembea ukubwani ama atahitaji mtu wa kumsaidia.
Meriam ambaye ameachiwa huru mapema wiki iliyopita na mahakama ya rufaa nchini humo, alihukumiwa kifo kwa madai ya kuikana dini yake ya kiislamu na kuwa Mkristo, lakini pia kosa lingine ni kufunga ndoa na mkristo jambo ambalo halitambuliwi na dini yake ya zamani kama ni ndoa halali bali ni uasherati hivyo anapaswa kuhukumiwa kifo.
Mwanamke huyo alikamatwa toka mwezi february mwaka huu na kuishi gerezani pamoja na mtoto wake mdogo wa kiume mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu. Baada ya shinikizo kutoka mataifa mbalimbali serikali ya nchi hiyo ilimwachia huru lakini akiwa na mumewe uwanja wa ndege wa Khartoum kuelekea nchini Marekani, alikamatwa tena na mumewe kwa madai ya kutumia hati za kusafiri za kufoji jambo ambalo kwa mujibu wa Meriam amelipinga kwamba si la kweli.
Meriam na mumewe Daniel Wani pembeni ni mtoto wao wa kiume.
Meriam na mumewe Daniel Wani wanauraia wa nchi mbili Marekani na Sudan ambapo Daniel anatumia hati ya kusafiria ya taifa la Sudan kusini jambo ambalo serikali ya Sudan imelipinga na kuwataka wote kutosafiri mpaka wamepata nyaraka halali za kusafiri, kitendo ambacho Meriam amekipinga akidai kwamba yeye na mumewe wana haki ya kutumia hati ya Sudan kusini kwakuwa mumewe ametokea huko. Kwasasa Meriam na familia yake wanakaa ndani ya jiji la Khartoum sehemu salama kwa mujibu wa Meriam ingawa hapana uhuru wa kutosha wakisubiri hati mpya za kusafiri.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni