Mwenyekiti wa DP, Mchungaji Christopher Mtikila akionyesha picha za X-Ray alizopigwa baada ya kupewa kipigo na watu wanaodaiwa kuwa ni wakazi wa Kurasini alipokwenda kuwahamisha Ijumaa iliyopita.
Dar es Salaam. Kiongozi wa Chama cha Democratic (DP), Mchungaji Christopher Mtikila amenusurika kifo na mtu mwingine aliyetambuliwa kwa jina moja la Mikidadi, ambaye yupo mahututi katika Hospitali ya Temeke, baada ya kushambuliwa na watu wanaodaiwa kuwa na mzozo wa ardhi eneo la Kurasini, jijini Dar es Salaam.
Mchungaji Mtikila alikumbwa na mkasa huo Ijumaa wiki iliyopita baada ya kufika katika eneo hilo kwa nia ya kutaka kuwaondoa watu hao wa familia tatu tofauti ambao wanaishi katika eneo hilo.
Kipigo hicho ambacho kimemsababishia majeraha ya kisogoni na hata kushonwa nyuzi tatu kichwani, kuvimba usoni na maumivu makali mwilini yalitokana na kipigo kutoka kwa familia mbili tofauti zinazoishi katika eneo hilo ambao wanapinga kuhama.
Pia katika sakata hilo, Mtikila anadai kupoteza simu mbili, pesa taslimu Sh400,000 na Dola za Marekani 2,000 na siku ya tukio na alifika hapo akiwa ameongozana na watendaji wa Dawati la Msaada wa Kisheria katika taasisi yake ya Liberty Fund International.
Kamanda wa Polisi Temeke, Engbert Kiondo alikiri kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa wanalifanyia uchunguzi na taarifa kamili itatolewa kesho Jumanne.
“Ni kweli suala hilo limeripotiwa hapa na tunalifanyia uchunguzi na kesho Jumanne nitatoa taarifa rasmi kwa waandishi wa habari,” alisema Kiondo.
Mtikila alisema, mara baada ya kufika eneo hilo, alikwenda katika nyumba ya kwanza na kuwakuta walinzi ambao walikubali na kuondoka katika eneo hilo kwani tayari notisi walikuwa nayo na walikuwa wanatambua kuwa wanatakiwa kuondoka.Alisema baadaye walikwenda katika nyumba ya pili ambayo anaishi mtu mmoja aliyemtaja kwa jina la Rubein Sanga ambaye hata hivyo vitu vyake vingi akuwa amekwisha vihamisha.
Alisema wakiwa mbele ya nyumba hiyo gari la polisi lilifika na wakiwa hawana hili wala lile vijana ambao anawataja kuwa ni wa Sanga walianza kuwashambulia kwa kutumia nondo na kila aina ya silaha za jadi.
“Walinipiga sana hadi nikapoteza fahamu na wakawa wanasema huyo Mtikila bebeni na mumchome moto, walitaka kuniua kwani walinikwida tai hadi ikakatika,” alisema.
Na kuitaja pia familia ya Evelyne Mboya kuwa ilishiriki kuwashambulia. Alisema wakati vurugu zinaendelea, ndipo akatokea mmoja wa jirani wanaoishi katika eneo hilo aliyemtaja kwa jina la Mikidaki: “Yule bwana alipojaribu kunitetea kuwa nisiendelee kupigwa alipigwa nondo kichwani na akaanguka na alishambuliwa hadi kuzirai na hajapata fahamu hadi leo,” alisema.
Mchungaji Mtikila alisema alikuwa ameambatana pia na walinzi wawili (mabaunsa), wafanyakazi wa dawati lake la msaada wa kisheria lililopo chini ya taasisi yake ya Liberty Fund International na mmiliki halali wa eneo hilo, Omar Salum Muhsin ambaye pia alijeruhiwa mkononi kwa nondo.
Mtikila aliwataja wafanyakazi wake waliojeruhiwa kuwa ni Hemed Wendo na Gray Mhando na akiwa amezirai alibebwa na kupandishwa katika gari hadi Kituo cha Polisi Chang’ombe ambako yeye na wenzake walifunguliwa jalada kwa shtaka la kuingia isivyo halali katika eneo la watu wengine.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni